
Afisa Habari wa Azam FC Jaffary Iddy Maganga amesema, wameondoka na baadhi ya wachezaji hii leo kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya kuweka kambi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara isipokuwa wachezaji waliokuwa timu ya taifa ya Tanzania pamoja na wachezaji wao na wale wa kimataifa.
Maganga amesema wachezaji wa timu ya taifa ambao ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Himid Mao, Salum Abubakary' Sure Boy' na John Bocco wataungana na wenzao Desemba sita kikosi kitakaporejea huku wa kimataifa wakiwa ni Allan Wanga aliye katika timu ya taifa ya Kenya, Didier Kavumbagu ambaye yupo timu ya taifa ya Burundi pamoja na Jean-Baptiste Mugiraneza aliye timu yake ya taifa ya Rwanda wataungana na timu kutegemea na matokeo katika michuano ya kombe la CECAFA Chalenji inayoendelea nchini Ethiopia.
Maganga amesema, wameamua kuweka kambi jijini Tanga kwa siku chache zilizobakia ili kukiweka kikosi imara kwa ajili ya muendelezo wa ligi kuu bara waweze kufanya vizuri zaidi kwa kuendelea kuwa vinara wa ligi kuu mpaka mwisho wa mashindano na waweze kuibuka mabingwa.