Friday , 2nd Dec , 2016

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya amewatolea uvivu wanafunzi wa elimu ya juu wanaodaiwa kujiuza kwa madai ya kukosa mkopo na kusema kuwa, wanafunzi hao wana tatizo la ziada na siyo mkopo pekee.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya akiwa Kikaangoni

 

Manyanya amefunguka hayo Jumatano hii alipokuwa katika kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka LIVE kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, ambapo alisema kukosa mkopo hakuwezi kuwa sababu ya mwanafunzi kufanya matendo yaliyo kinyume na maadili na kusisitiza kuwa hiyo ni tabia ya mtu na kwamba serikali isitwishwe mzigo huo.

"Kama kweli kuna wanafunzi wa kike wanaojiuza kwa kukosa mkopo, wana tatizo la ziada, haiwezekani hiyo iwe sababu, maana kama ni kukosa mkopo wanafunzi wengi wanakosa, mbona wengine hawafanyi hivyo? na je wanafunzi wa kiume wanaokosa mkopo wao wauze nini?" alihoji Manyanya na kuwaonya waache mara moja tabia hiyo.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao na kuwafundisha maadili mema ili wasiwe na tabia za aina hiyo ambazo ni kinyume na mila za kitanzania, pamoja na kuwagharamia masomo yao.

"Wazazi lazima wajue wajibu wao ni pamoja na kuwasomesha waototo wao, wasitegemee kila kitu serikali, serikali ina nafasi yake na wazazi wana nafasi yao, ni lazima wawajibike"

Amesema kwa wanafunzi waliokosa mikopo na hawana uwezo watafute njia nyingine ikiwa ni pamoja na kutumia ndugu jamaa na marafiki kwa kuwa hakuna mwaka ambao wanafunzi wote walipata mkopo huku akiwataka watambue kuwa mkopo ni msaada na ni kitu cha ziada hivyo si cha kutegemea sana.

Tags: