Thursday , 15th Oct , 2015

Kitendo cha muziki wa sasa kuwa wa kibiashara zaidi, ni moja ya sababu inayopelekea wasanii wengi kutoandika na kuimba nyimbo za kuwaenzi waasisi mbali mbali wa Taifa.

Taariza hiyo imetolewa na msanii Kala Jeremiah alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa radio, na kusema kwamba wasanii wengi hawaimbi nyimbo hizo kwa kuwa wanafanya muziki kibiashara zaidi.

"Nadhani watu wengi wameenda kwenye mlengo wa biashara sasa ukiimba wimbo utakaomuingizia pesa, sasa mara nyingi ukiimba wimbo ambao una maono kama hayo hauwi sana kibiashara, japokuwa watu wengi wanapenda kusikia nyimbo kama hizo, sasa siwezi kujua kwa nini wasanii wengi hawawezi kuimba nyimbo kama hizo, lakini mi nahisi wanaangalia kuangalia nyimbo ambazo zimekaa kibiashara", alisema Kala.

Kala aliendelea kusema kwamba wasanii na watu mbali mbali kwenye jamii wanatakiwa kuwaenzi waasisi wetu kwa nafasi yake, kwani ndio walipigania taifa kufika hapa.

"Inatakiwa tukumbuke pia upande wa pili, kwa sababu hawa ni watu ambao walitupigania, ni watu ambao waliishi maisha ya shida kwa ajili yetu, kwa hiyo nadhani hata tunapoadhimisha siku ya kumkumbuka baba wa Taifa, nadhani tujaribu kumuenzi kwa kila mmoja na nafasi yake", alisema Kala.

Pia Kala Jeremiah ameitaka serikali kuitangaza nyumba ya makumbusho ya Mwalimu Nyerere iliyoko kijijini Mwitongo Wilayani Butiama, kwani ina mambo mengi ambayo Watanzania wengi hawayafahamu.