Msanii Nay wa Mitego akiwa na Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza amesema kuwa wamemfungulia msanii Nay wa Mitego kuendelea na sanaa baada ya kutekeleza maagizo aliyopewa ikiwa pamoja na kuomba msamaha kwa jamii, kukiri kubadilika ila bado wameendelea kuufungia wimbo wake wa 'Pale kati' kwani bado hauna maadili kwa jamii licha ya msanii huyo kuufanyia marekebisho mara mbili.
"Tumemfungulia Msanii Nay wa Mitego kwa kutekeleza maagizo aliyopewa, kujutia na kukiri kubadilika. Wimbo wa 'Pale Kati' bado haukidhi. Pamoja na kuufanyia marekebisho mara mbili wimbo wa Pale Kati bado haukidhi. Tunaendelea kuufungia hadi itakapoelekezwa vinginevyo, tunatoa maelekezo kwa vyombo vya habari kutocheza wimbo wa 'Pale Kati'. Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekaidi" Amesema Mngereza
Mbali na hilo msanii Nay wa Mitego ametangaza kuachia wimbo mwingine mpya ambao unaweza kutoka wiki hii.