Kituo cha East Africa Television (EATV) na East Africa Radio leo hii kimezindua rasmi kampeni yake kubwa ijulikanayo kama #ZamuYako2015, yenye lengo la kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu kufanya maamuzi katika michakato mitatu muhimu kwa mustakabali wa taifa katika mwaka huu.
Akizindua kampeni hiyo leo Jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Mkuu wa Vipindi wa East Africa Radio, Nasser Kingu ameitaja michakato hiyo kuwa ni kujiandikisha katika daftari la kuduma la wapiga kura, kupiga kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa pamoja na kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Amesema walengwa ni vijana wenye umri wa miaka 18 mpaka 40 ambao ni watanzania milioni 15,293,681 idadi ambayo ni sawa na asilimia 68.20 ya watu wenye sifa ya kupiga kura nchini Tanzania ambao ni milioni 22,424,136.
Kingu amewataka watanzania hasa vijana kuacha dhana ya kutotoa ushirikiano kwenye maswala muhimu yanayotoa maamuzi kitaifa kwakuwa madhara ya kutoshiriki ni makubwa kwa taifa hasa kurudisha nyuma maendeleo ya nchini.