Monday , 2nd Feb , 2015

Waajiri nchini wametakiwa kutoa fursa kwa wauguzi na wauguzi wakunga kujiendeleza kitaaluma kwa elimu ya masafa wakati wapo kazini, ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika utoaji wa huduma.

Waajiri nchini wametakiwa kutoa fursa kwa wauguzi na wauguzi wakunga kujiendeleza kitaaluma kwa elimu ya masafa wakati wapo kazini, ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika utoaji wa huduma, sambamba na kukabiliana na wahudumu wa afya katika vituo vya kutolea huduma.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa chuo cha wauguzi kilichopo Mirembe mkoani Dodoma, Anna Shemangula, wakati akizungumza na EATV kuhusiana na mafunzo yanayoendelea chuoni hapo, sambamba na katika vyuo vingine kumi nchini kwa wauguzi na wauguzi wakunga wa ngazi ya cheti, wanaojiendeleza katika elimu ya diploma.

Bi Anna amesema katika uendeshaji mafunzo hayo, pamoja na mafanikio mengi wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wauguzi kushindwa kujiendeleza wakiwa kazini, ukosefu wa vifaa kama kompyuta za kujisomea majumbani na baadhi ya waajiri kuwanyima fursa wafanyakazi wao ya kujiendeleza hata wanapoipata nafasi.

Meneja miradi wa kujenga uwezo kutoka shirika la AMREF Africa, wanaoendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na wizara ya afya, kwa ufadhili wa mashirika mbalimbali likiwemo la GSK, amesema mradi huo umesaidia kupunguza tatizo la utoaji wa huduma za afya hasa vijijini.

Ameongeza kwamba sambamba na mradi huo wana mpango mwingine wa ufadhili wa  mafunzo ya muda mrefu kwa vijana wanaotoka familia za kawaida,wanaomaliza kidato cha nne  kutoka maeneo yenye matatizo makubwa ya huduma za afya kama vile Simiyu, Shinyanga, Lindi, Mtwara na Tanga..