Thursday , 14th Jan , 2016

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja au nyingine, wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu; na sasa linawasiliana na wamiliki wa taasisi za kifedha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro amesema wameanza kuweka ulinzi mkali katika benki mbalimbali, ikiwemo zilizopo eneo la Mlimani City na kwamba wanakagua pikipiki na watu wanaowatilia shaka.

Kamanda Sirro amesema wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja ama nyingine wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu, na kutokana na hilo, watawahoji wafanyakazi wa taasisi za fedha nchini ili kubaini ni nani wanaohusika.

“Tumeanzisha oparesheni maalumu dhidi ya pikipiki ambao wanavunja sheria barabarani na wanaojihusisha na masuala ya uhalifu jijini,’’ alisema Kamanda Sirro ambaye ameshika wadhifa huo kuanzia Januari mosi mwaka huu''“

Kamanda Siro ameongeza kuwa jeshi hilo limekamata pikipiki 150 kwa Mkoa wa Kipolisi Temeke, 241 Kinondoni na Ilala 249 ambazo baadhi yao zimelipiwa faini na nyingine zinachunguzwa kuona uhalali wake.