Friday , 3rd Mar , 2017

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Mwansasu ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kuongea na vijana wa kike ikiwa ni pamoja  na kuwaweka wazi juu ya  njia mbalimbali za kujisitiri pindi wanapoanza kuona mabadiliko katika miili yao.

Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson

Leo katika kipindi cha East Africa Breakfast, wakati akizungumzia  kampeni ya 'Namthamini' inayoendeshwa na EATV LTD kuelekea Siku ya Wanawake Duniani  Dkt. Tulia amesema kwamba jamii nyingi hazina utaratibu wa kuongea kwa uwazi mabinti kutokana na mila potofu zilizopo katika makabila tofauti nchini.

“Kuna makabila ni mwiko mzazi kuzungumza na binti yake kuhusu masuala ya ukuaji hivyo hata mama kumfundisha binti namna ya kujisitiri kwa njia za kienyeji ni tabu, hapo ndiyo ambapo unamkuta binti anaona bora asiende shule abaki nyumbani mpaka siku za mzunguko wake wa hedhi utakapoisha”. Alisema Dkt Tulia

Pamoja na hayo Dkt. Tulia amekiri umasikini upo juu na hicho ndicho chanzo cha wanafunzi wengi kushindwa kumudu gharama za taulo hizo (Pedi), na kuongeza kuwa kwa maeneo ya vijijini taulo hizo hazipo jambo ambalo linawafanya mabinti wengi kutumia vifaa ambayo kiafya ni hatari.

Dkt. Tulia ameongeza kwamba jukumu la mzazi yoyote yaani baba au mama ni kuhakikisha vijana wanawekwa wazi kinapofika kipindi cha hedhi na balehe, siyo kuendeleza mila potofu ambazo zinaleta madhara kwa baadae ikiwa ni pamoja na kutimiza majukumu ya kifamilia kama kumuandalia binti vifaa vya kujisitiri na siyo kuiachia serikali kwa sababu jambo hilo likiachiwa serikali halitokuwa endelevu.

Hata hivyo Naibu Spika amesema kuwa ipo mijadala ya aina hiyo mingi ikiitaka bunge liweke mjadala wa kuishawishi serikali ishughulike na jambo hilo moja kwa moja lakini mijadala hiyo itafanyika kwa kipindi kifupi na siyo endelevu.

“Hili jambo lisiachiwe serikali pekee nashauri, kwa kuwa litafanywa kwa muda mfupi sana halitakuwa endelevu, lakini naomba liwe jukumu la kila mzazi kwamba mzazi anavyoona chakula, mavazi, madaftari ni jukumu basi unapokuwa na mtoto wa kike akianza mabadiliko ya mwili na umri ukiwa umesogea bajeti ya taulo za hedhi kila mwezi inabidi uzitambue kama ni jukumu lako" - Dkt. Tulia.

Pamoja na hayo ameipongeza East Africa Television Limited kwa kuja na kampeni hiyo ambayo imeamsha hisia za watu wengi kuanza kuwajali mabinti na pia imewezesha watu kufahamu  changamoto wapatazo watoto wa kike wawapo mashuleni.

Dkt Tulia Ackson