Friday , 30th May , 2014

Jumla ya wagonjwa wapya milioni 3.4 huugua saratani za mfumo wa chakula na ini na kati yao wengi wanatoka katika nchi masikini ikiwemo Tanzania.

Makamu wa rais wa Tanzania, Dkt Mohammed Gharib Bilal.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakati akifungua kituo cha Tiba, Uchunguzi na Mafunzo ya Magonjwa na Saratani za Tumbo pamoja na Ini katika hospitali ya taifa Muhimbili na kuongeza kuwa wastani wa watu 30-35 kati ya watu laki moja hufariki dunia kila mwaka kwa saratani ya koo la chakula.

Naye Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Nchini Tanzania Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema kituo hicho kitatoa huduma za upasuaji, kufungua koo la chakula lilizoziba kwa kansa na zile za kubadilisha viungo vya ndani kama ini huku Mwenyekiti wa bodi ya udhamini ya hospitali hiyo Dkt. Gabriel Uponda akisema kituo hicho kina madaktari nane wenye uwezo wa kutoa huduma za matibabu hayo.