Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Akizungumza na balozi wa Ujerumani nchini hivi karibuni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema moja ya matatizo yanayoikabili Zanzibar ni vijana wengi kukosa ajira na shughuli za kujiletea maendeleo hivyo Ujerumani ina nafasi kubwa ya kupambana na jambo hilo.
Kwa upande wake balozi wa Ujerumani nchini Egon Kochanke, amepokea maombi hayo na kuongeza kuwa anaelewa Zanzibar inazo fursa muhimu za kiuchumi na biashara ikiwemo kilimo cha viungo na utalii ambazo wawekezaji wa ujerumani wanaweza kuzitumia katika kufungua miradi.
Wakati huo huo, Baraza la Taifa la Biashara TNBC limewataka watendaji wa Halmshauri nchini kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuweza kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni mkoani Iringa na katibu mtendaji wa baraza hilo Raymond Mbilinyi wakati akiongea na wajumbe wa baraza hilo la mkoa huo juu ya mikakati ya kuimarisha uchumi na kujenga mazingira bora ya biashara katika mkoa huo.
Mbilinyi amesema kuwa baraza hilo litaunganisha sekta binafsi na sekta za umma kuhakikisha wanafanya kazi pamoja na hivyo ni jukumu la watendaji wa ngazi za juu katika halmashauri hizo kujenga mazingira bora ya biashara ili kuvutia wawekezaji.