Monday , 15th Jun , 2015

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaban Bin Simba amefariki dunia leo katika hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam.

Akithibisha kutokea kwa kifo hicho, Kaimu Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni Mh Mary Nagu amesema msiba huo umetokea leo asubuhi na kwamba marehemu alikuwa akisumbulia na kisukari na shinikizo la moyo kwa muda mrefu.

Mh. Nagu amesema serikali inaungana na waislamu wote kuomboleza msiba huo, na kumuelezea marehemu kwamba alikuwa ni kiungo muhimu kati ya waislamu na serikali.

Amesema taratibu nyingine zinashughulikiwa na Baraza la Waisilamu Tanzania BAKWATA ambao watatoa taarifa rasmi muda wowote hii leo

Taarifa za kifo hicho pia zimethibitishwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhadi Mussa Salum, ambaye ameeleza kuwa taarifa zaidi atazitoa baadae.

Sheikh Salum amesema kuwa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu itafanyika kesho majira ya saa nne asubuhi ambapo waisilamu wote watakusanyika kabla ya kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao Shinyanga.

Akimuelezea marehemu, Sheikh Salum amesema Mufti alikuwa ni mstahimilivu na mvumilivu wa hali ya juu kwa maana licha ya kukumbana na vizingiti vingi, bado aliweza kusimama na kuiimarisha BAKWATA.

Wakati wa uhai wake Mufti Bin Simba alikuwa akisumbuliwa kwa muda na maradhi ya shinikizo la damu na kisukari.