Akizungumza na wadau wa mazingira kutoka maeneo kame nchini kwenye semina iliyofanyika mjini Singida, Mkurugenzi wa kituo cha mafunzo ya Tabia Nchi cha chuo kikuu cha Dar es salaam Prof. Pius Yanda amewataka wananchi kutumia changamoto za mabadiliko ya Tabia Nchi kama fursa za maendeleo na kuachana na kilimo cha mazoea.
Watafiti wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, mhadhiri Dkt. Emma Liwanga na mtaalam wa mazingira Bw. Edmund Mabhuye wamesema lengo la mradi ni kuboresha maisha ya jamii inayoishi katika maeneo kame kwa kuibua njia za kukabiliana na hali hiyo kutoka kwa wakazi wa maeneo husika.
Nao baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamesema juhudi kutoka kwa serikali pamoja na wadau wa mazingira zinahitajika kufikisha elimu kwa wananchi ili kuwasaidia wakulima na wananchi kwa ujumla kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi na kupunguza madhara yatokanayo na hali hiyo