Katibu mkuu kiongozi balozi Ombeni Sefue amekiri kuwepo kwa mapungufu katika mfumo wa ufuatiliaji wa tathmini ya fedha na rasilimali za serikali hali inayochangia kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na utendaji mbovu katika idara na taasisi za serikali kwenye utoaji huduma kwa umma huku miradi mingi ya maendeleo hasa kutoka kwa wahisani kusitishwa kwa sababu ya vitendo hivyo.
Balozi Sefue amebainisha hayo katika mkutano wa faragha wa makatibu wakuu manaibu katibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa ambapo amesema mapungufu hayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kuzorotesha utoaji huduma kwa umma pamoja na kukwamisha shughuli za maendeleo na kuonya kuwa serikali imechoka kuvumilia matukio hayo na kiongozi yeyote atakayekosa dhamira ya kuyakomesha atawajibishwa.
Balozi Sefue pia amesema katika kuhakikisha viongozi wanawajibika ipasavyo kwa jamii serikali hivi sasa inafanya upembuzi yakinifu wa kuanzisha kituo cha tathmini ya uongozi ili utumishi wa umma uwe chachu ya maendeleo ya taifa licha ya mpango huo kuonekana kupigwa na baadhi ya viongozi.
Awali katika mkutano huo mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi amewataka watumishi wa umma kuzingatia welendi katika kutekeleza majukumu yao badala ya kusubiri kusukumwa na matamko au maagizo kutoka ngazi za juu za uongozi kama ilivyokuwa hivi sasa kwa agizo la Rais la ujenzi wa maabara Tatu katika kila shule ya sekondari.