Tuesday , 23rd Oct , 2018

Baraza la Mitihani Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya Darasa la saba kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2018 ambapo matokeo hayo yameongezeka kwa asilimia 4.96 ukilinganisha na matokeo ya mwaka jana.

Katibu Mtendaji NECTA Charles Msonde

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Taifa Charles Msonde ufaulu umetajwa kuongezeka kwenye masomo ya hisabati, sayansi, maarifa ya jamii ambapo katika masomo hayo somo la kingereza limeelezwa kuwa na ufaulu wa chini ya asilimia 50 ukilinganisha na masomo yote.

Dk. Charles Msonde amesema “tathmini ya awali kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 4.9% ikilinganishwa na 2017, pia kiwango cha ufaulu wa somo la Kiingereza uko chini sana tofauti na masomo mengine, chini ya asilimia 50."

Aidha amesema “baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa zaidi 100 kutokana na kuugua kipindi cha mtihani na kuwapa fursa ya kufanya mtihani huo mwaka 2019 pamoja na kutangaza kuyafuta matokeo ya wanafunzi 357 kwa makosa ya udanganyifu."

Jumla ya watahiniwa 733,103 kati ya 943,318 wamefaulu mtihani huo wa kuhitimu elimu ya msingi uliofanyika septemba 5 na 6 mwaka huu sawa na asilimia 77.72 kati yao wasichana 382, 273 na wavulana 350,273.