Baadhi ya waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Marehemu Nasra Mvungi katika uwanja wa jamhuri Morogoro, muda mfupi kabla ya maziko.
Mamia ya wakazi wa manispaa ya morogoro wakiwemo viongozi wa serikali, asasi za kiraia viongozi wa dini na kijamii wamekusanyika katika uwanja wa jamhuri mjini morogoro kuuaga mwili wa mtoto nasra mvungi aliyefariki dunia baada ya kuteswa na kufichwa kwenye boksi na mama yake mkubwa kwa miaka minne baada ya kufariki kwa mama yake mzazi na kukosa haki za msingi kama mtoto.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera na mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdulaziz Abood wamewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa na kutoa wito kwa wananchi na viongozi wa serikali kuwa na utaratibu wa kutembeleana na kujua matatizo yanayozikabili familia ikiwa ni pamoja na kubaini maovu kama yaliyofanywa kwa mtoto Nasra.
Naye Slamu Mposo kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu(LHRC) amelaani vikali vitendo vya kinyama kama hivyo vinavyoendelea nchini na kuahidi kuwa watahakikisha wanatoa ushirikiano sehemu yoyote ambapo kuna vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama alivyofanyiwa mtoto nasra, ili sheria ichukue mkondo wake.
Wananchi waliokusanyika katika uwanja huo leo wamelaani vikali vitendo kama hivyo na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kuiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao.
Tayari walezi hao na baba mzazi wa mtoto Nasra, Rashid Mvungi, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kumfanyia ukatili kwa kumtesa mtoto huyo.
Mvungi ambaye ni baba mzazi yupo nje kwa dhamana, na ameweza kufika katika uwanja wa jamhuri kuuaga mwili wa mtoto wake, huku wakitarajia kurudishwa mahakani kwa mara nyingine tarehe 9 mwezi huu.