Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamini Mkapa
Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa amewataka wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokubali kuruhusu chokochoko za kikabila, kisiasa na kidini zinazoweza kuleta machafuko na kupelekea mauaji ya kimbari kwani ni jambo linalowezekana.
Akizungumza na vijana kutoka nchi mbali mbali za jumuiya ya Afrika Mashariki katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika Arusha. Rais mstaafu Benjamini mkapa amesema wananchi hasa vijana wanaweza kuziba mianya yote ya machafuko, lakini pia wanaweza kuwa chanzo cha machafuko kama tahadhari hazitachukuliwa.
Katika hatua nyingine Rais mtaafu Benjamini Mkapa ameishauri Jumuiya ya Afrika Mashariki kuijengea uwezo mahakama ya Afrika kwani ina nafasi kubwa ya kusaidia kudumisha amani katika ukanda wa nchi hizo.
Awali katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mshariki Dkt. Richard Sazbera amewataka viongozi na wananchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuyachukulia mauaji ya kimbari ya Rwanda kama chanzo cha kuepuka machafuko na kudumisha amani
Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wakiwemo mabalozi, na wabunge wa Jumuiya hiyo yalianza kwa maandamano yaliyopita katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha