Friday , 23rd Nov , 2018

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam imemfutia dhamana Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko baada ya kujiridhisha juu ya viongozi hao kukiuka masharti ya dhamana.

Ester Matiko (mbele kulia), Freeman Mbowe (katikati) na John Mnyika (kushoto)

Uamuzi huo wa mahakama umetolewa leo na Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri wakati kesi ya vigogo saba wa CHADEMA ikisikilizwa, ambapo leo ilikuwa ni siku ya kutoa uamuzi juu ya dhamana kwa watuhumiwa wawili ambao ni Freeman Mbowe na Ester Matiko.

Ester Matiko na Mbowe walikuwa wakituhumiwa kutumia vibaya kibali cha dhamana yao baada kushindwa kuhudhuria kufika mahakamani zaidi ya mara 1  bila ya kuomba ruhusa ya mahakama.

Freeman Mbowe alitajwa kusafiri kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua, huku Ester Matiko akitajwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali.

Kufuatia maamuzi hayo ya mahakama huenda viongozi wao wawili wakarudishwa rumande mpaka pale  kesi yao itakuwa inasikilizwa.

Licha ya uamuzi huo wa mahakama wa kuwafutia dhamana viongozi hao wawili, wakili wa upande wa  utetezi, Peter Kibatala amebainisha kuwa watakata rufaa kwenye mahakama ya rufani.

Mbowe na viongozi 6 wa CHADEMA wanakabiliwa na makosa 13 ikiwemo kosa la kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)  Akwilina Akwilini pamoja na kosa la uchochezi.