Tuesday , 4th Aug , 2015

Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania CCM, kimesema kuwa kura za maoni sio hatua ya mwisho ya kuteuliwa kuwa mwakilishi wa kugombea katika jimbo lakini vikao vya juu vya chama hicho ndio vitatoa maamuzi ya Mwisho juu ya Mgombea.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi (CCM), Nape Moses Nnauye.

Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam Katibu mwenezi wa Chama hicho Ndugu, Nape Nnauye amesema kuwa mchakato huo utaangaliwa na kamati kuu kwa kuwa sehemu nyingine uligubikwa na Udanganyifu katika upigaji wa Kura.

Nnauye ameongeza kuwa Wagombea wa Chama hicho wanaohisi wameonewa katika mchakato huo wasubiri maamuzi ya Kamati kuu ambayo inafatilia jinsi zoezi hilo lilivyoendeshwa ili kuweza kutoa haki kwa kila Mwanachama wa chama hicho.

Aidha Nape ameongeza kuwa Chama hicho kitaendelea na ratiba zake kama kawaida ambapo mpaka tarehe 13 mwezi huu ndipo watatoa majina ya wagombea watakao wakilisha majimbo na kata katika Uchaguzi mkuu wa mwezi Octobar.

Kuhusu kutetereka kwa chama kutokana na kuhamwa na makada wake akiwemo aliewahi kuwa Waziri Mkuu Mh. Edward Lowassa na wengineo Nape amesema kuwa Chama hicho bado kipo imara na wana uhakika wa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.