Tuesday , 23rd Jun , 2015

Kamanda wa polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabas, amesema tuhuma alizotoa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kuwa jeshi lake linamwonea kwa kumkamata na kumweka ndani hovyo, wakati yeye siyo mwahalifu.

Kamanda wa polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabasi.

Akizungumza leo kwa njia ya simu ya kiganjani, amesema kuwa Lema anasababisha vurugu kwa kutembelea maeneo ambayo watu wamejitokeza na kujiandikisha na kuanza kupiga hotuba kitu ambacho kinyume cha sheria.

Amesema Mh. Lema amekuwa chanzo cha vurugu katika uandikishwaji wa daftari la wapiga kura kwenye BVR.

Sabas amesema kuwa jeshi la polisi haliwezi kuonea mtu wala yeye Mbunge, isipokuwa likipata taarifa kama siku ya tukio ya Juni 20 alipokamatwa kuwa analeta vurugu na wananchi hawataki kumwona katika maeneo ya uandikishaji ndipo walipokwenda kumkamata.

Amesema siku ya tukio walipata taarifa toka kwa askari walioko doria kwenye kituo cha olsunyai kuwa kuna vurugu toka kwa Mbunge na kuomba ulinzi uongezwe na askari wakapelekwa zaidi na kumtia mbaroni na wenzake 24 na kuwa jumla ya watuhumiwa 25 walikamatwa na siyo yeye aliyetoa taarifa polisi kuomba ulinzi.

Pia amemtuhumu Lema kuongozana na kundi la watu toka maeneo tofauti na uandikishwaji, kitu ambacho siyo sahihi pia na ambacho kinakera baadhi ya watu.

Hata hivyo uchunguzi dhidi ya tuhuma zake zinaendelea na upelelezi ukikamilika atachukuliwa hatua stahiki.

Awali Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, aliyekamatwa amelilalamikia jeshi la Polisi, kwa kumkamata na kumuweka mahabusu masaa mawili na nusu jana, wakati akiwa kwenye kata ya Olsunyai Manispaa ya Arusha,
akizungukia waandikishwaji wa daftari la wapiga kura, ili kujionea hali halisi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema amesema kuwa ameshangazwa na kitendo hicho kwani yeye ndiye aliyewaita polisi ili kumsaidizi ulinzi katika kituo cha olsunyai, baada ya kuvamiwa kwa kupigwa mawe na kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa wa kundi la mgombea ubunge wa chama cha CCM.

Amesema walikaa ndani Juni 20 mwaka huu, kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa 4:00 usiku na kuwataka wajidhamini wenyewe, kisha kuwaachia.

Lema amesema yeye ni kiongozi na sheria inamtaka ahamasishe watu kujitokeza na kujiandikisha na inapobidi kutoa elimu, lakini, hapaswi kudhalilishwa kwa kuwekwa mahabausu kwa kejeli na dharau.