Wednesday , 13th Jan , 2016

Halmashauri ya Wilaya ya chamwino Mkoani Dodoma imepokea jumla ya tani 1,620 za chakula cha msaada kutoka serikalini kati ya tani 14,300 zinazohitajika ili kukabiliana na tatizo la njaa katika Wilaya hiyo.

Wanakijiji katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma wakiwa wanashughulikia Mlo wao kutokana na baa la Njaa

Taarifa hiyo imetolewa leo na mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Saada Mwaluka wakati akizungumza na East Afrika Radio kuhusiana na kiasi cha chakula cha msaada ambacho Wilaya hiyo imepokea ili kukabiliana na njaa.

Mwaluka amesema kuwa katika awamu ya kwanza Halmashauri hiyo ilipokea jumla ya tani 150 na katika awamu ya pili halmashauri hiyo ilipokea jumla ya tani 1,470 ambazo zimeshagawiwa kwa watu.

Amesema katika awamu ya pili ambayo jumla ya tani 1,470 zimetolewa, tani 1,000 zitauzwa kwa bei nafuu ya sh. 50 kwa kilo huku tani 470 zitagawiwa bure kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na wazee.