Sunday , 6th Apr , 2014

Rais Jakaya Kikwete leo amewaongoza wakazi wa jimbo la Chalinze mkoani Pwani kupiga kura kumchagua mwakilishi wao katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Rais Jakaya Kikwete akipiga kura yake katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Msoga, kata ya Msoga,Chalinze Mwaka 2010.

Wakazi wa jimbo la Chalinze mkoani Pwani wamepiga kura kumchagua mwakilishi wao katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania huku Rais wa jamhuri ya
muungano wa Tanania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe mama Salma
Kikiwete wakiwa ni miongoni mwa wapigakura walioshiriki katika zoezi hilo
wapikipiga kura yao katika kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi msoga
ambapo ndipo yalipo makazi yao.

Majira ya saa tatu na nusu asubuhi Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe mamaSalma Kikwete waliwasili na kuingia kituoni hapo wakifuata utaratibu wa
kawaida ambapo mama Salma alikuwa wa kwanza kuingia ndani ya kituo na kupiga kura yake akifuatiwa na Rais Kikwete ambaye baada yakumaliza zoezi hilo amezungumza na waandishi wa habari.

Vituo vingi katika maeneo ya jimbo la Chalinze vimeonekana kuwa na watu
wachache waliojitokeza kupiga kura majira ya asubuhi huku kukiwa na
malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea hasa wa vyama vya upinzani
waliolalamikia jinsi mwenendo mzima wa uchaguzi ulivyokuwa ukiendelea huku
mgombea wa CCM Ridhiwan kikwete kwa upande wake akisema kuwa hana
malalamiko kwakuwa alikuwa hajapita vituoni.

Akizungumzia malalamiko hayo ya baadhi ya wagombea msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Chalinze Samuel Salianga amesema hajapokea malalamiko kutoka kwa mgombea au chama chochote cha siasa lakini utaratibu wa watu wanaokutwa na
kasoro za majina katika shahada na daftari la wapigakura wanaweza kujaza
fomu inayowaruhusu kutumia haki yao ya kupiga kura.

Uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Chalinze umefanyika kufutia kifo cha
aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Saidi Bwanamdogo aliyefariki
Januari 22 mwaka huu ambapo vyama vitano vya siasa vya AFP NRA, CHADEMA, CCM na CUF
vimeshiriki uchaguzi huo na matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa
kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa na zoezi la kuhesabu kura na
kutangaza mshindi wa kiti hicho litafanyika katika ofisi ya muda ya tume ya
uchaguzi iliyopo katia shule ya sekondari Chalinze.