Wednesday , 29th Aug , 2018

Waziri Mkuu wa Jamhuyri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa leo amekagua ujenzi wa barabara za juu (Flyover) katika eneo la Tazara jijini Dar es salaam na kujiridhiha na hali inavyoendelea akibainisha kuwa zipo katika hatua ya mwisho kukamilika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akiangalia barabara za juu katika eneo la Tazara.

''Hii ndio kasi tunayoitaka kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara za juu na hapa Tazara naona umekamilika kwa asilimia 98 hivyo mwezi Oktoba mwaka huu tunatarajia itafunguliwa na Rais Dkt. John Magufuli'', amesema.

Aidha Waziri Mkuu amebainisha kuwa lengo la mradi huo wa barabara ya juu chini ya ufadhili wa Serikali ya Japan, ni kupunguza msongamano wa magari katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, hivyo ilibidi uende haraka ili kutatua kero hiyo kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi Mkoa wa Dar es Salaam watafute eneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo ili waweze kuondoka kandokando ya barabara hizo za juu zinazojengwa ikiwemo ile ya Ubungo ambayo ipo katika hatua za awali.

Barabara za Mandela na Nyerere hukutanisha abiria wanaotoka maeneo ya mjini kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na wengine huelekea Temeke.