Jumamosi , 30th Mei , 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewataka watanzania wote nchini wajenge tabia ya kuandika wosia ili kuondoa matatizo ya mirathi pindi mume anapoaga dunia.

Waziri Mkuu Mizengo wa Tanzania Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda.

Ametoa wito huo wakati akizindua kampeni ya kuandika wosia kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia uandishi wa wosia mbele ya wakili, Waziri Mkuu alisema uandishi wa wosia ni suluhisho la migogoro mingi inayosababishwa na wanandugu ambao wakati mwingine wala hawakushiriki kuchuma mali wanayogombea.

“Kuandika wosia siyo uchuro kama ambavyo watu wengi wanadhani… ninatoa wito kwa watanzania kuandika wosia mapema kwani inasaidia kuondoa matatizo ya mirathi baada ya mmoja wao kuondoka duniani,” alisema.

“Mtua anapaswa kutamka mali nilizonazo ni kadhaa na endapo nitakufa mali hii apewe fulani, na hii fulani na nyingine fulani. Hati hii inapaswa kutunzwa kwa mwanasheria, benki au kwa Kabidhi Wasii. Tusipolifanya hili, matatizo yataendelea kuwakumba wajane na watoto walioachwa na marehemu,” alisema.

Alipoongeza TAWLA kwa kuchukua jukumu la kuhamasisha umma kuhusu suala la uandishi wa wosia lakini pia akawataka wanachama wa TAWLA wajikite zaidi kwenye kutetea haki za makundi maalum kama walemavu wa ngozi, vikongwe na watu kutoka makabila madogodogo. “Haya makundi yana shida zao ambazo hazifanani na watu wengine. Nendeni vijijini, mkatoe elimu, jueni changamoto wanazokabiliana nazo, wasikilizeni shida zao na muone ni njia gani mnaweza kuwasaidia,” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka nane kuanzia mwaka 2006 hadi 2014, jumla ya vikongwe 2,219 waliuawa katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mara, Kagera na Mwanza ambayo alisema yote iko Kanda ya Ziwa. “Mauaji haya yanasababishwa na imani potofu za kishirikina; jamii kuwa na uelewa mdogo wa sheria; ukosefu wa imani za kiroho; ukosefu wa elimu; na waganga wa kienyeji kupiga ramli,” alisema.

Alisema makabila madogo yanakabiliwa na matatizo ya ardhi ambayo ndiyo tegemeo lao kuu, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi wanatishiwa usalama wa maisha yao bila sababu yoyote. “Nendeni mkatoe elimu zaidi kwa watu hawa ili tuwalinde wazee wetu, makabila madogo kama Wahadzabe na Wasandawe pamoja na ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa TAWLA, Bi. Aisha Bade alisema chama hicho kimetumia wanasheria wanawake zaidi ya 200 na wasaidizi wa kisheria 400 (paralegals) kutoa msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali ambao hawana uwezo kumudu gharama za kesi.

“Katika mwaka 2014, tumetoa msaada wa kisheria kwa watu zaidi ya 10,000 ambao hawana uwezo kumudu gharama za kesi kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini,” aliongeza.

Naye Balozi wa Sweden nchini, Bw. Lennarth Hjelmaker, akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo nchini alisema Serikali ya nchi hiyo ilitenga kiasi cha sh. bilioni 4 kusaidia mpango wa miaka minne wa chama hicho wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usawa wa kijinsia.

“Hadi sasa tumekwishatoa sh. bilioni 3.5 ambazo kati ya hizo, sh. bilioni 1.1 zimetumika kusaidia wanawake wapatiwe haki zao; sh. milioni 500 zimetumika kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya ili watoe huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana na sh. milioni 700 zimetumika kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya chini wanaohusika kutoa maamuzi. Kiasi cha sh. bilioni 1.2 kimetumika kuendeleza shughuli za chama,” alifafanua.

Pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kutetea haki za akina mama na wasichana, Balozi huyo wa Sweden alisema kuna haja ya kuweka mkazo ili kuwafikia wanaume na wavulana wengi zaidi ili waweze kujirekebisha na kubadili tabia na mitazamo yao dhidi ya wanawake na wasichana.