Akizungumza na East Africa Radio, mmoja wa wadau wa soka nchini Paul Makoye amesema, Kocha Mart Nooij alishafeli akiwa Timu ya Taifa nchini Msumbiji lakini bado Tanzania tumeendelea kuwa naye bila kujua ya kuwa timu inazidi kufanya vibaya.
Makoye amesema, kocha huyo anatakiwa kuondoka mara baada ya kumaliza michuano ya COSAFA ambayo Timu ya Taifa Stars imeshindwa kuendelea mbele baada ya kufungwa na timu ya taifa ya Madagascar bao 2-0.
Stars ilianza michuano hiyo vibaya baada ya kufungwa na Swaziland bao 1-0 katika mchezo wake wa kwanza ambapo kufuatia taifa Stars kupoteza michezo yote miwili, inaungana na Lesotho kutoka kundi B kuaga michuano hiyo, huku kundi A timu za Mauritius na Shelisheli zikiwa zimeshaaga michuano hiyo pia.
Katika hatua hiyo, TFF inatarajiwa kukutana katika kikao cha kamati ya utendaji Mei 24 mwaka huu ili kupokea na kujadili mienendo, maandalizi na maendeleo ya timu za taifa za mpira wa miguu nchini.