Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini Johnson Minja akiwa mahakamani
Minja alifikishwa leo kwenye mahakama ya wilaya ya Dodoma ambapo amesomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili ambapo hata hivyo alikana mashtaka yote mawili ya uchochezi yanayomkabili.
Akisoma mashtaka mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Dodoma, Rhoda Ngimilanga mwendesha mashtaka wa serikali, Paul Kadushi ameiambia mahakama hiyo kuwa mnamo Septemba 6 mwaka 2014 mshtakiwa akiwa katika chuo cha mipango kilichopo kata ya Miuji Manispaa ya Dodoma alitoa kauli zilizochochea kutendeka kwa kitendo cha jinai kinyume na sheria namba 390 kifungu cha 35 na 16 vilivyofanyiwa marekebisho.
Aidha katika kosa la pili siku hiyohiyo mshtakiwa alitenda kosa kwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kuwachochea wafanyabiashara nchini kutotumia mashine za kielektroniki za kukusanya kodi (EFDs).
Hata hivyo Minja amekana mashtaka yote yanayomkabili ambapo baada ya wakili huyo wa serikali kumsomea maelezo ya awali yanayomkabili kuna baadhi ya maelezo aliyakubali na mengine aliyakataa.
Maelezo aliyoyakubali ni pamoja na kukiri mahakamani hapo kuwa kuna sheria ya matumizi ya mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukusanyia kodi, sheria ya kukusanya kodi pamoja na kukiri utambulisho wake uliotolewa mahakamani hapo.
“Pia ni kweli kuwa Septemba 6 mwaka 2014 tulifanya mkutano katika chuo cha mipango kilichopo kata ya Miuji katika manispaa ya Dodoma kwa lengo la kuwapa wafanyabiashara mrejesho wa maendeleo ya mazungumzo yetu na TRA juu ya matumizi bora ya EFDs ili kuiongezea serikali mapato bila kuua uchumi wa nchi na mfanyabiashara mwenyewe,” alisema Minja
Ameongeza kusema kuwa, “Pia kwenye mkutano huo tuliteua wajumbe kwenda kwenye kamati ya pamoja.”
Hata hivyo aliyakataa maelezo ya mwendesha mashtaka wa serikali kuwa katika mkutano huo alitoa kauli za uchochezi.
Baada ya maelezo hayo hakimu Ngimilanga aliwauliza upande wa serikali kama wameshawaandaa mashahidi katika kesi hiyo ambapo wakili huyo wa serikali alisema kuwa wana zaidi ya mashahidi 15 pamoja na vielelezo ambapo wataviwasilisha mahakami hapo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 8 mwaka huu ambapo itasikilizwa kwa muda wa siku tatu mfululizo hadi Juni 10 ambapo upande wa serikali utaleta mashahidi wanne kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi hiyo.