Jumapili , 7th Dec , 2025

“Ushahidi uliobakia ukikamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata".

Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe limethibitisha kuwa linawashikilia Isakwisa Lupembe na Ally Mwafongo, wakazi wa mji wa Tunduma na kukanusha uvumi uliosambaa mtandaoni kuhusu kutekwa kwao na watu wasiojulikana.

Taarifa iliyotolewa leo Disemba 7 na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, SACP Augustino Senga imesema kuwa Isakwisa Lupembe na Ally Mwafongo, walikamatwa kama sheria zinavyoelekeza na wanaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kushiriki katika makundi ya mtandaoni yanayohamasisha watu kuandaa na kusambaza taarifa za uongo, uzushi, uchonganishi, kujenga chuki na nyinginezo kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

“Ushahidi uliobakia ukikamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata,” taarifa hiyo imeongeza.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia uhuru wa kujieleza kwa kukiuka sheria za nchi kwani kufanya hivyo athari zake ni kwa wote wanaojengewa chuki na wanaosambaza taarifa hizo za uongo, uzushi, uchonganishi na kujenga chuki katika jamii.