Jeshi la Polisi Nchini limesema linaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya usalama nchini na kutoa tahadhari kali kwa makundi na watu binafsi wanaotoa kauli, matangazo au mikutano inayoweza kuhatarisha amani.
Katika taarifa iliyotolewa leo Novemba 21,2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dodoma, jeshi hilo limesema “halitasita kuchukua hatua dhidi ya makundi na watu binafsi wanaotoa kauli, matangazo au mikutano inayoweza kuhatarisha amani na kuibua chuki miongoni mwa wananchi, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria”
“Jeshi la polisi linatoa tahadhari kuwa halitasita kuchukua hatua dhidi ya mambo kama hayo yenye lugha laini na nyingine kali zenye uchochezi”taarifa hiyo imeongeza.
Jeshi la Polisi limesema litaendelea kuchukua hatua kwa matamko na matendo yote yenye lengo la kuchochea chuki na vurugu nchini wakati huu ambao nchi ikiwa na jukumu kubwa la kuleta maridhiano ili kulinda amani na utulivu na kuendelea kukuza uchumi na kuongeza kuwa kukitokea vurugu kila mmoja ataathirika hasa kiuchumi, kijamii na kiusalama.

