Jumanne , 14th Oct , 2025

Rais Donald Trump amethibitisha kuwa atamkaribisha Volodymyr Zelenskiy White House Ijumaa hii kujadili msaada wa kijeshi na makombora ya Tomahawk, huku Urusi ikionya kuwa hatua hiyo ni uchokozi mkubwa dhidi yake.

Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Zelenskiy kutangaza kuwa anasafiri kuelekea Washington kwa mazungumzo muhimu kuhusu ulinzi wa anga na uwezo wa mashambulizi ya masafa marefu wa Ukraine.

Akizungumza akiwa njiani kurejea kutoka Mashariki ya Kati, Trump alisema, "Nadhani ndiyo, tutakuwa naye hapa Ijumaa,” akithibitisha ziara hiyo itakayolenga kujadili mustakabali wa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine. 

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika ombi la Kyiv la kupatiwa makombora ya Tomahawk, yenye uwezo wa kufika hadi Moscow — hatua ambayo Urusi imeitaja kuwa ni uchokozi mkubwa.

Zelenskiy alisema tayari amempa Trump maelezo kuhusu idadi ya makombora wanayoyahitaji, akisisitiza kuwa mazungumzo ya kina yatafanyika ana kwa ana. 

Amesema anatarajia kujadili pia hatua za kuimarisha ulinzi wa anga wa Ukraine, hasa baada ya mashambulizi mapya ya Urusi kwenye jiji la Kharkiv, yaliyoharibu kituo cha afya na kukatiza umeme katika wilaya tatu.

Ziara hii inatarajiwa kuwa kipimo muhimu cha uhusiano kati ya Kyiv na Washington chini ya uongozi wa Trump, hasa katika kipindi hiki ambacho Marekani inachunguza kwa kina usawa wa msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine na athari zake kwa usalama wa Ulaya.