
Ajali iliyotokea baada ya basi la Kampuni ya Mallesa lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Geita kugongana na lori la mizigo katika Kijiji cha Rumasa, Wilaya ya Chato, mkoani Geita imeua watu wawili.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kwa njia ya simu kuwa watu wawili wamefariki dunia ambao walikuwa katika gari dogo la mizigo aina ya Canter lililokuwa likitoka Jijini Mwanza kuelekea wilayani Kibondo mkoani Kigoma likiwa limebeba vifaa vya ujenzi.
“Ni kweli ajali imetokea na watu wawili waliokuwa ndani ya gari la mizigo wamepoteza maisha,” alisema Kamanda Jongo, na kuongeza kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea ambapo ameahidi kutoa taarifa kamili baada ya taratibu za kiuchunguzi kukamilika.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema tukio hilo limetokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo, Oktoba 7, 2025.