Mwenyekiti mpya wa CHADEMA Tundu Lissu akihutubia wajumbe leo hii 22 Januari, 2025
Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake ametangazwa kuwa mshindi wa kiti cha Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) akipata kura 513 (51.5%) akiwashinda wapinzani wake Freeman Mbowe ambaye ameshika nafasi hiyo kwa miaka 21 amepata kura 482 (48.3%) na Odero Odero amepata kura moja tu (0.1%).
Kwenye nafasi ya Makamu wa Rais wa chama hicho John Heche ametangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo kwa upande wa bara akipata kura 577 akiwashinda wapinzani wake Ezekia Wenje aliyepata kura 372 na Mathayo Gekul aliyepata kura 49 tu.
Na kwa upande wa Zanzibar Said Mzee Said ametangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Zanzibar akipata kura 625 za ndiyo kati ya kura 706 huku akipata kura 75 pekee za hapana na kura zilizoharibika ni sita mara baada ya uchaguzi wa Makamu wa Rais kwa Zanzibar kurudiwa kwasababu wagombea wote hawakufikisha angalau asimilia 50 ya kura za halali zilizopigwa.
Tundu Lissu anahitimisha utawala wa Mwenyekiti aliyepita Freeman Mbowe wa miaka 21 tangu mwaka 2004 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kwenye nafasi hiyo aliyoachiwa na Bob Manyanga Makani ambaye alihudumu kwa awamu mbili pekee.