Basi la abiria likiwa limepinduka katika moja ya ajali ambazo chanzo chake kikitajwa kuwa ni uzembe wa madereva.
Baadhi ya kanuni hizo ni pamoja na pendekezo linalompa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, mamlaka ya kuwalazimisha madereva wazembe, kwenda kozi ya mwaka mmoja katika vyuo vya mafunzo ya udereva, iwapo watabainika kuwa wamehusika kusababisha ajali za makusudi.
Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Johansen Kahatano, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo na kufafanua kuwa hatua hiyo itahusisha pia kushusha daraja la leseni ya dereva husika.
Akifafanua zaidi kuhusu kanuni hizo ambazo bado hazijaanza kutumika, kamishna Kahatano amesema kwa kiasi kikubwa zitasaidia kurejesha nidhamu ya matumizi ya sheria za usalama barabarani kwani zitaenda sambamba na matumizi ya aina nyingine za adhabu kwa makosa ya usalama barabarani zinazotolewa hivi sasa.
Ameongeza kuwa dereva anapohitimu masomo hayo ya lazima, atatakiwa kuanza upya kuomba leseni ya udereva na hata atakapoipata ataanzia daraja la chini kabisa na sio lile alilofikia kipindi alipobainika kufanya makosa.
Aidha, Kahatano amesema kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa madaraja ya leseni ya udereva yatatolewa baada ya dereva kuhitimu mafunzo, akiwa na maana kuwa madereva watatakiwa kwenda kusoma kabla ya kuomba kupandishiwa madaraja ya leseni zao.