Hukumu hiyo imetolewa leo Novemba 20,2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ndeko Dastan, baada ya kusikiliza mashahidi watano wa Jamhuri akiwemo mhanga na kujiridhisha pasi na kuacha shaka kwamba mtuhumiwa ametenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo, mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo Agosti 16, 2024, katika maeneo ya kijiji cha Shilima, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Mhanga ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kisheria, alifanyiwa kitendo hicho wakati ameagizwa na mama yake dukani na wakati anarudi ndipo mtumiwa alimvuta nyuma ya nyumba ya baba wa mhanga kisha kumfanyia ukatili huo.
Mshtakiwa ameiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye mwenyewe ni mgonjwa wa mapafu, ana watoto watano mmoja mlemavu na pia anamlea mdogo wake ambaye naye ni mgonjwa pia mkewe amemuachia mzigo mkubwa wa kulea hiyo familia ni kubwa.
Mshtakiwa licha ya kuomba Mahakama impunguzie adhabu, Hakimu Ndeko amesema kwamba mahakama hiyo imefungwa mikono kwani kifungu cha 131 (3) cha kanuni ya adhabu ambacho mtuhumiwa ameshtakiwa nacho kinatoa adhabu ya kifungo cha maisha na hakijampa Hakimu kubadili adhabu hiyo.