Jumatatu , 11th Dec , 2023

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kutambua nafasi yake katika matumizi ya bima ya afya kwa wote na kuzingatia upatikanaji wa bidhaa za afya, ubora na bei zilizo katika muongozo wa matibabu wa serikali.

Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk.Grace Magembe

Maagizo hayo yalitolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk.Grace Magembe wakati akifungua kikao cha MSD na wateja wake wakubwa.  

Katika kikao kazi hicho Dk.Grace amesisitiza MSD kuhudumia wananchi kutokana na mahitaji na taasisi zote za afy kuangalia mifumo ya utoaji huduma inavyoweza kubadilika kukidhi mahitaji ya bima ya afya kwa wote.

“Tuangalie upya mifumo yetu ya utoaji huduma namna inavyoweza kubadilika ili kukidhi mahitaji ya bima ya afya kwa wote.Tusisumbue wananchi muwasiliane wenyewe wao wanataka hudum," amesema

Kwa mujibu wa Dk.Grace alifafanua kuwa muswada wa bima ya afya umepitishwa kinachoendelea sasa ni kufanyia kazi kanuni kwakushirikiana na mwanasheria mkuu wa serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu,Wizara ya Fedha,Ikulu na wadau wengine.

Kwa upande wake Mfamasia  Mkuu wa Serikali Daud Msasi alisema, kikao hicho kitajadili changamoto na kutafuta  suluhuhisho ili MSD aweze kuwahudumia wateja wakubwa kwa bidhaa wanazozihitaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai alisema, lengo la kuwakutanisha wateja wakubwa ni kwa sababu mahitaji yao ya dawa ni makubwa tofauti na hospitali nyingine.