Jumanne , 29th Aug , 2023

Afrika Kusini, Urusi na China zimempongeza Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kufuatia ushindi wake wa uchaguzi uliokumbwa na utata mwishoni mwa wiki.

Wakati huo huo, Marekani imeongeza sauti yake kwa ukosoaji mkubwa wa uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita ambao upinzani uliuelezea kama "udanganyifu". Serikali ya Marekani imesema kulikuwa na upendeleo wa kimfumo dhidi ya upinzani na kuonyesha ripoti za kuaminika kwamba wachunguzi walilazimika kubadilisha baadhi ya fomu za matokeo ya uchaguzi. Tume ya uchaguzi imekanusha madai hayo.

Taarifa kutoka ofisi ya rais wa Afrika Kusini imesema Afrika Kusini inafahamu kuwa uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira magumu ya kiuchumi kutokana na vikwazo dhidi ya Zimbabwe.Pia imekiri wasiwasi kutoka kwa waangalizi huru wa uchaguzi kuhusu uhalali wa matokeo.

Baadhi ya wachunguzi wanasema uchaguzi huo ulikosa viwango vya kimataifa na matakwa ya katiba ya Zimbabwe.

Afrika Kusini, Urusi na China ni washirika muhimu wa kibiashara wa Zimbabwe, na uungaji mkono wao katika uchaguzi huo ni muhimu wakati Zimbabwe inakabiliwa na uwezekano wa kutengwa zaidi na mataifa ya magharibi baada ya ukosoaji wa uchaguzi huo.

Muungano wa Wananchi wa upinzani wa Mabadiliko bado unahesabu matokeo yake kabla ya kuamua juu ya mpango thabiti wa nini cha kufanya baadaye. Lakini ujumbe wa pongezi kwa Rais Mnangagwa labda ni kielelezo kwamba washirika wakuu wa Zimbabwe wako tayari kuendelea na kukubali matokeo.