
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa Demokrasia uliofanyika leo Agosti 22, 2023 jijini Dares salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Comrade Abdurahman Kinana amesema anaamini uchaguzi ujao utafanyika kukiwa na muafaka wa jumla na maelewano yanayokidhi mahitaji ya uchaguzi huru na wa haki.
"Msingi wa mjadala wa Katiba nadhani ni ule alioueleza rais wakati anaondoa katazo la mikutano ya hadhara, alisema hivi tusijifunge kwenye waraka wowote, tutaangalia mema yaliyoko kwenye Katiba ya sasa, tutaangalia ya kwenye mapendekezo ya Warioba na pia Katiba pendekezwa" amesisitiza Comrade Kinana
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema kwa kuwa maoni, mazungumzo na mawazo mbalimbali namna ya kuendeleza mchakato huo yameshafanyika, kwa sasa hakuna budi kujadili muafa wa kitaifa ili katika mkutano wa Bunge la mwezi Septemba, muswada wa kuendeleza mchakato wa katiba utakaojibu matatizo ya kidemokrasia upelekwe kujadiliwa.
"Lazima kwanza tupeleke bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya nchi vile vifungu vyote vile tunavyotaka virekebishwe, virekebishwe kwenye Katiba, muswada urudi kwa rais ausaini uwe sheria ya marekebisho ya Katiba" - John Mnyika.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Hashim Rungwe amesema matatizo ya demorasia ya uchaguzi nchini yanatokana na mazonge ya kuwa na Tume ya Uchaguzi ambayo haipo huru toka mwanzo wa mandalizi ya uchaguzi mpaka wakati wa kutoa matokeo.
"Sisi tunpata shida kwasababu ya mazongo tuliyonayo, tunapaswa kuwa na tume huru ambayo toka mwanzo itakuwa tume huru kweli kweli na isiwe na mazongo mengine, mimi nafikiri wananchi wanahitaji tume huru, tume ambayo haipati maelekezo kutoka huko juu" - Hashim Rungwe.
Mkutano huo wa siku mbili wa wadau wa Demokrasia nchini umefanyika jijini Dar es salaam ikiwa ni uelekeo wa kutafuta muafaka wa pamoja utakaokidhi matakwa ya Uchaguzi Huru na Haki.