Alhamisi , 25th Dec , 2025

Mahakama hiyo imemuhukumu Iddi Nassoro kutumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya huku ikiwaachia huru wenzake watatu.

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemtia hatiani Mshtakiwa Iddi Nassoro kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.02 ndani ya Stendi ya Magufuli Mbezi akisafirisha kuelekea mkoani Tanga.

Kufuatia kosa hilo, Mahakama hiyo imemuhukumu Iddi Nassoro kutumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya huku ikiwaachia huru wenzake watatu.

Hukumu hiyo ya Mahakama imetolewa Disemba 24 mbele ya Jaji Godfrey Isaya baada ya mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili na kuona upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha shtaka la kusafirisha dawa za kulevya pa sina kuacha shaka dhidi ya mshtakiwa wa pili.

Jaji Isaya alisema Mahakama iliona upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa kwanza Maliki Maliki, Ally Jafari Maliki ambaye ni Kocha wa Mpira wa Miguu na Mwingi Mgazija Mwinyi hivyo iliwaachia huru.

Washtakiwa katika shauri hilo walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili ambapo katika shtaka la kwanza kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza Maliki Maliki, wa pili Iddi Nassoro na mshtakiwa wa tatu Ally Jafari Maliki ambao walidaiwa Machi 24 mwaka 2022 maeneo ya Stendi ya Magufuli Mbezi walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.02 kuelekea mkoani Tanga.