Jumamosi , 29th Jul , 2023

Mabaki yamepatikana baada ya helikopta ya jeshi la Australia kuanguka katika pwani ya Queensland, na kuwaacha watu wanne wakiwa hawajulikani waliko, polisi wamesema.

Tukio hilo lilitokea wakati wa mazoezi ya Marekani na Australia katika kisiwa cha Lindeman Ijumaa usiku.

Waziri wa ulinzi Richard Marles amesema operesheni ya utafutaji na uokoaji ilizinduliwa mara moja.
"Wafanyakazi wanne wa ndege bado hawajapatikana," Marles alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumamosi asubuhi. Alisema kuwa helikopta ya MRH-90 Taipan ilianguka karibu na kisiwa hicho .
"Matumaini yetu na mawazo yetu ni mengi sana kwa ndugu na familia zao," alisema, akiongeza kuwa "tuna matumaini makubwa ya habari bora wakati wa mchana".Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Angus Campbell amesema ni "huu wakati wa kuogofya".

"Lengo letu kwa sasa ni kutafuta watu wetu na kusaidia familia zao na timu yetu yote," alisema.
Alisema anashukuru msaada uliotolewa na mashirika ya kiraia, polisi, umma na "washirika wetu wa Marekani" kusaidia operesheni ya utafutaji na uokoaji hadi sasa.