Jumatatu , 3rd Jul , 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema Wizara yake imejipanga kufanya mageuzi kwenye sekta ya mifugo Morogoro kwa kuanzisha programu ya kuwawezesha vijana na wafugaji wengine kufanya ufugaji wa kibiashara na kuifanya sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa wa kipato.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, wakati akizungumza na viongozi kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima

Waziri Ulega ameyasema hayo wakati akiongea na viongozi wa mkoa wa Morogoro na kusema mkoa huo una fursa nyingi zinazoweza kuinua uchumi wa wananchi wake kwa kutumia uzalishaji wa mifugo ikiwemo ardhi nzuri inayowezesha kupatikana kwa maji ya uhakika na malisho kwa mifugo.

"Mkuu wa mkoa, Wizara yangu imepanga kutenga eneo lenye ukubwa wa hekta 10,000 kutoka kwenye Ranchi mama kwa ajili ya vijana waliomaliza mafunzo kwenye vituo atamizi na wafugaji wa mkoa wa Morogoro ambao wanahitaji maeneo ya malisho (Livestock Guest House) kwa ajili ya kufanya unenepeshaji wa mifugo," amesema Waziri Ulega

Alifafanua kuwa katika maeneo hayo watakayoyatenga kwa ajili ya kupangisha wafugaji kwa muda mfupi wataiwekea  miundombinu kama vile majosho, mabwawa, mabilika, mazizi, ghala la majani na nyumba maalum ya mifugo.

Aidha, aliongeza kuwa serikali itaendelea kutoa elimu ya uwekezaji kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya mifugo kwa wadau wote wakiwemo wafugaji huku akiwataka wafugaji kumiliki maeneo  kwa ajili ya mifugo yao.

Halikadhalika, alisema ili kukabiliana na migogoro, Wizara kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Morogoro pamoja na wadau wa sekta ya mifugo imepanga kumega jumla ya hekta 27,006.27 kwa ajili ya kuwapatia  wananchi wa vijiji vya Twatwatwa, Parakuyo, Ngaite, Tindiga A na B, huku akisisitize kuwa maeneo hayo yagawiwe vizuri na yatumike kwa shughuli zilezile za Mifugo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema kuwa ana imani kubwa na Wizara na aliiomba kuingia makubaliano rasmi na mkoa huo katika kufanya programu za ufugaji wa kibiashara  ili wananchi wa mkoa huo wanufaike na ufugaji na kuepuka migogoro isiyo na tija.

Aliongeza kuwa wanataka kuanzisha vituo vya BBT mifugo mkoani humo vingi iwezekanavyo ili vijana na wafugaji wengine wapate elimu ya ufugaji wa kibiashara waweze kujikwambua kimaisha.