Awali mchezo huo wa fainali ulikuwa umepangwa kufanyika kesho kwenye dimba la Uwanja wa Taifa, lakini kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TTF imepelekea mchezo huo kuhamishiwa Chamazi.
Mchezo huo wa fainali utaanza saa 10 kamili jioni.
Bingwa wa Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza atazawadiwa Kombe pamoja na medali, huku mshindi wa pili akipata kikombe na medali pia.
Viingilio vya mchezo huo ni tsh.5,000 kwa jukwaa kuu na tsh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.
Wakati huo huo, Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea leo (Jumamosi) katika viwanja vitatu tofauti, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ndanda FC ya Mtwara watawakaribisha Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga katika mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Ngwanda Sijaona.
Huku wakata miwa wa Kagera Sugar wanaoutimia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakiwakaribisha Maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mjini Morogoro timu ya Polisi.
Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea tena kesho jumapili katika viwanja vitatu tofauti, Uwanja wa Chamazi wenyeji Azam FC wataikaribisha timu ya maafande wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania Prisons, mchezo utakaonza majira ya saa 2 kamili usiku.
Mjini Shinyanga wenyeji timu ya Stand United wataikaribisha Simba SC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku wagonga nyundo wa jiji la Mbeya, timu ya Mbeya City wakicheza na timu ya Young Africans kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.