Jumatano , 9th Nov , 2022

Miili saba ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, ikiwemo familia moja ya mume na mke waliofariki kwa ajali ya gari la kubebea wagonjwa siku ya Novemba 7, 2022 imesafirishwa kwa ajili ya mazishi.

Miili ya watumishi saba wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto

Halmashari ya wilaya ya Kiteto imegharimia mazishi hayo kwa kusafirisha miili hiyo pamoja na familia kupatiwa kiasi cha shilingi 700,000 kama ubani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto, John Nchimbi, katika tukio la kuaga miili hiyo ametaja maeneo itakapopelekwa na kuzikwa miili hiyo.

Mwili wa Joseph Bizuru Thomas (35) muuguzi daraja la I umesafirishwa kwenda wilaya ya Igunga Tabora, Agapiti Kimario Clemence (32)  mwalimu daraja la II utazikwa Moshi Tarakea pamoja na mwenzi wake Catherine Asenga Thadei (31) muuguzi daraja la I.

Mwingine ni Selina Andrea Nyimbo (29) mtechnolojia msaudizi daraja la I, Nickson Damian Mhomwa (36) Tabibu daraja la I aliyepelekea Iringa Kilolo.

Kididi Saidi Athumani (33) muuguzi daraja la I mwili wake umepelekwa Mikese Morogoro na Edward Edwine Makundi (50) daktari daraja la I ambaye mwili wake umepelekwa Marangu Moshi kuzikwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Carolina Mthapula, akiongoza kuagwa miili hiyo aliwatoa hofu wananchi wa Kata ya Sunya kuwa atahakikisha Kituo cha Afya Sunya kinaongezewa watumishi kwa ajili ya huduma hiyo kwa wananchi.