
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifunga Mkutano wa Mawakili wa Serikali uliofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma.
Waziri Dkt. Ndumbaro amewataka Mawakili hao kuandaa orodha ya kesi zote za madai zilizo kwenye taasisi zao, chanzo na sababu ya kesi hizo, taarifa hiyo ieleze gharama au hasara ambayo Serikali inaweza ikaingia, na taarifa iseme ni nani amesababisha kesi hiyo kwa jina na cheo chake, na taarifa hizo za kesi ziwasilishwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Pia, amewaeleza Mawakili wote wa Serikali wajiandae kuelimisha umma kuhusu Katiba tuliyonayo na haki za binadamu ili kujenga uelewa kwa wananchi na kupata hoja zao badala ya kupata hoja kutoka kwa wanasiasa pekee hasa tunapoelekea kuwa na katiba mpya ikizingatiwa kuwa haya ni maelekezo ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, Chama Tawala kinachoongoza Serikali ya Awamu ya Sita iliyopo madarakani chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan.