Jumatano , 28th Jan , 2015

Wazabuni mbalimbali wa vyakula wametanganza kuwa ifikapo Februari 1 mwaka huu endapo serikali itakuwa imeshindwa kuwalipa deni la zaidi Bilioni 2 watasitisha kutoa huduma ya vyakula katika taasisi mbalimbali za serikali.

Katibu Tawala Mkoa wa mara bw Benedict Ole Kuyani.

Akitoa tamko baada ya kumalizika kwa kikao chao cha pamoja mjini Musoma, katibu wa wazabuni hao mkoa wa Mara Mwita Wambura, amesema licha ya kuwasilisha madai yao katika taasisi hizo za majeshi ya polisi, magereza, vyuo vya ualimu na afya pamoja na shule za sekondari lakini serikali imeshindwa kulipa deni hilo, hatua ambayo imewafanya kukosa mitaji ya kuendelea kutoa huduma hizo…

Nao baadhi ya wazabuni hao wameonesha kusikitishwa na kitendo cha serikali kukaa kimya kwa kushindwa kuyapatia ufumbuzi madai hayo na kufanya wengi wao sasa kuaanza kuuziwa nyumba zao ambazo waliweka kama dhamana katika taasisi za mbalimbali za fedha na hivyo wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za kuwalinda wafanyabiashara wa ndani ambao wamekuwa wakitoa huduma katika taasisi hizo za serikali .

Akizungumzia madai hayo kwa njia ya simu Katibu Tawala Mkoa wa Mara bw Benedict Ole Kuyani, amesema halmashauri za wilaya zinahusika na uendeshaji wa shule za sekondari na wizara husika za taasisi hizo ndizo zinazowajibika kulipa na kuzungumzia madai hayo na juhudi za kutafuta wasemaji wa wizara bado zinaendelea.