Jumapili , 25th Jan , 2015

WANAWAKE nchini wametakiwa kutokuwa na imani potofu pamoja na uoga katika michezo hususani mchezo wa mpira wa magongo.

Akizungumza na East Africa Radio, Mmoja wa wachezaji aliyehitimu mafunzo ya ukocha wa mchezo huo, Kidawa Suleiman amesema kumekuwa na upungufu mkubwa wa wanawake katika mchezo wa mpiara wa magongo suala linalorudisha nyuma mchezo huu hususani katika kuunda timu ya wanawake hapa nchini itakayoweza kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Kidawa amesema, suala la kutokujitokeza kwa wanawake ili kujifunza mchezo huu kunachangia pia kushindwa kuunda timu mpya ambazo zitaweza kusaidia kwa ajili ya kuweza kuukuza na kuutangaza mchezo huu nchini.

Kwa upande wake mmoja wa wachezaji wa timu ya mpira wa magongo ya wanaume, Samson Lusaulwa amesema, mchezo huu unasaidia kutoa fursa ya ajira kwa watu wote iwapo atakuwa makini katika mafunzo ya mchezo huu.

Lusaulwa amesema, kozi ya makocha kwa Tanzania ni jambo la muhimu ambalo linaweza kusaidia kupata makocha wengi na wenye uwezo ambao watagawanyika katika mikoa mbalimbali pamoja na kuandaa ligi ya mchezo huu wa mpira wa magongo Tanzania ili kuweza kupata timu nzuri ya Taifa ambayo itaweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya nje ya nchi.