
Baadhi ya wanachama wa CHADEMA wakiwa mahakamani
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kufanya ghasia katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kawekamo jimbo Kuu la Mwanza, Agost 15, 2021, na kusababisha waumini wa kanisa hilo kushindwa kusikiliza neno la Mungu.
Kesi hiyo namba 77 ya mwaka 2021, ilifunguliwa Oktoba 19, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo na tangu wakati huo washtakiwa hao hawakuwahi kusomewa maelezo ya awali ya kesi yao na kuishia kupigwa kalenda hadi leo hii yaliposomwa mahakamani hapo.
Wakili wa serikali, Gisela Banturaki, ameiambia mahakama hiyo kwamba siku ya tukio wanachama hao walivaa mavazi ya chama chao yaliyoandikwa katiba mpya ambayo yalisababisha waumini washindwe kusikiliza neno la Mungu na kuanza kuwaangalia ndipo viongozi wa kanisa hilo wakawaita na kuwataka watoke nje ili wakabadilishe mavazi hayo, lakini walikaidi.
Wakili huyo ameongeza kuwa baada ya kukaidi agizo la viongozi wa kanisa, waliitwa polisi kwa ajili ya kuwakamata ambapo baada ya kuwakamata waliwapeleka katika kituo cha polisi cha kati cha jijini Mwanza.
Kesi hiyo ambayo ipo chini ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Bonaventure Lema, upande wa mashtaka unatarajia kupeleka mashahidi saba wakiwamo viongozi wa dini wa kanisa hilo na vielelezo vinne vya ushahidi.
Washtakiwa wote19 wamekana mashtaka yao yanayowakabili.