Jumapili , 13th Feb , 2022

Mabingwa wa ulaya Klabu ya Chelsea usiku wa jana ilishinda ubingwa wa klabu bingwa ya Dunia kwa kuifunga klabu ya Palmeiras ya Brazil magoli 2-1 kwenye fainali iliyopigwa kwa dakika 120.

Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich

Ubingwa huo umeifanya Chelsea kufikisha makombe 21 walioshinda chini ya umiliki wa Roman Abramovich tangu June mwaka 2003.

Takribani miaka 19 imepita tangu bilionea raia wa Urusi Roman Abramovich alipoinunua klabu ya Chelsea Mwezi June mwaka 2003 kutoka kwa Ken Bates ambae baadae alienda kuinunua klabu ya Leeds United.

Wakati Abramovich anainunua Chelsea ilikuwa haijashinda ubingwa wa Ligi Kuu England kwa takribani miaka 50 mara ya mwisho walikuwa wameshinda msimu wa 1954-55, lakini toka hapo chini ya utawala wake klabu hiyo imeshinda ubingwa wa Ligi hiyo mara 5, na ubingwa wa usiku wa jana umeifanya Chelsea kufikisha jumla ya makombe 21 chini ya uwekezaji wake.

Chelsea imeshinda makombe yote kwa daraja la klabu chini ya bilionea huyo wameshinda ubingwa wa Ligi kuu England mara 5, Kombe la FA mara 5, ubingwa wa kombe la Ligi (Carabao Cup) mara 3, Ligi ya mabingwa barani ulaya (UEFA Champions League) mara 2 ubingwa wa Europa League mara 2, Ngao ya Jamii mara mara 2, Ubingwa wa UEFA Super Cup 1 na ubingwa wa klabu bingwa Dunia mara 1.

Lakini mafanikio haya ya Chelsea kwenye utawala wa Ramon Abramovich yamepatika akiwa amefanya kazi na makocha 15 tofauti akiwemo kocha wa sasa Mjerumani Thomas Tuchel ambaye ameshinda makombe 3 ndani ya kipindi cha mwaka 1, lakini Kocha Jose Mourinho ameifundisha Chelsea kwa vipindi viwili tofauti na ameshinda jumla ya makombe 8 akiwa na The Blues.