Ijumaa , 12th Dec , 2014

Jumla ya watanzania milioni 11,491,661 sawa na asilimia 62 ya matarajio yaliyowekwa wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Khalist Luanda

Aidha mkoa wa Dar -es-salaam umetajwa kufanya vibaya katika zoezi la uandikishaji huku mkoa wa Katavi ukiongoza kwa kufanya vizuri nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusiana na kukamilika Kwa zoezi la uandikishwaji wa daftari la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Khalist Luanda amesema katika zoezi hilo walitarajia kuandikisha wapiga kura wapatao milioni 18,587,742.

Amesema licha ya zoezi hilo kufanikiwa kwa zaidi ya nusu ya malengo ipo mikoa 2 na halmashauri mbili ambazo hazikufikia malengo na kuandikisha chini ya asilimia 50.

Ametaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam ambao uliandikisha asilimia 43 ya wapiga kura na mkoa wa Kilimanjaro ambao uliandikisha asilimia 50 ya wapiga kura.

Kwa upande wa halmashauri zilizofanya vibaya ni Kilindi iliyopo mkoani Tanga ambayo imeandikisha asilimia 21 na Halmashauri ya Wilaya ya Same iliyoandikisha asilimia 22.

Luanda ametaja mikoa miwili iliyofanya vizuri kuwa in Katavi ambao umevuka lengo Kwa kuandikisha asilimia 79 na ule wa Kagera ambao umevuka lengo Kwa kuandikisha asilimia 78 ya wapiga kura.

Ametaja halmashauri zilizofanya vizuri kuwa ni Mpanda ambayo imeandikisha asilimia 107 na kuvuka lengo pamoja na wilaya ya Babati ambao umeandikisha asilimia 101 ya wapiga kura na kuvuka lengo.

Akielezea utaratibu utakaotumika wa kupiga kura amesema ili kuthibitisha kuwa jina lililopo katika orodha ndilo la muhusika anayekuja kupiga kura watatumia vitambulisho aina nane ikiwemo cha kupigia kura, cha kazi, leseni na pasi ya kusafiria.

Ameviomba vyama vya siasa kutumia siku zilizobaki za kampeni kuhamasisha wanachama wao kujitokeza kupiga kura ili mafanikio yaliyopatikana katika zoezi la uandikishaji liende sambamba na upigaji kura na kusisitiza kuwa suala la ulinzi limeimarishwa.