Jumamosi , 1st Mei , 2021

Mabingwa watetezi wa kombe la Shirikisho Tanzania FA Cup Simba SC watashuka dimbani leo Saa 1:00 Usiku uwanja wa Mkapa kucheza dhidi ya Kagers Sugar katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano hii.

Mchezaji wa Simba Luís Miquissone akishangilia goli kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar

Kuelekea mchezo huu wekundu wa msimbazi wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele kwenye michuano hii kutokana na mwenendo bora wa kikosi hicho msimu huu ukilinganisha na Kagera Sugar ambao hawajawa na matokeo mazuri.

Kagera hawajashinda mchezo hata mmoja kwenye michezo 10 ya mwisho waliocheza wakati Simba wameshinda michezo 7, wametoka sare michezo miwili na wamefungwa mchezo mmoja kwenye michezo 10 ya mwisho kwenye michuano yote.

Lakini pia hata rekodi zinaibeba zaidi Simba kwenye michezo waliokutana na wanankurukumbi, katika michezo mitano ya mwisho Simba wameshinda mara nne wakati Kagera wameshinda mchezo mmoja.

Mchezo mwingine utakao chezwa leo, Dodoma jijini watakuwa wenyeji wa timu kutoka Manispaa ya Kinondoni KMC, mchezo huu utachezwa katika dimba la Jamuhuri Dodoma kuanzia majira ya Saa 10:00.