Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Bwana Willison Kabwe
Baadhi ya Wabunge wameomba mwongozo wa kutaka kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Bwana Willison Kabwe kutokana tuhuma kuipatia kazi kampuni ya Tanzania Buildings Works ambayo imeshindwa kutekeleza miradi ya ujenzi katika mikoa yote aliyoiongoza ikiwemo Mbeya na Mwanza na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni Tatu.
Akiomba mwongozo wa spika kufuatia kauli ya waziri wa ujenzi Dkt John Magufuli wa kutaka kuchunguzwa kwa kampuni hiyo, Mbunge wa Rombo Mhe. Joseph Selasini amesema mkurugenzi huyo chini ya uongozi wake ndio ametoa kazi kwa kampuni hiyo ambayo alipohamishiwa mkoani Mwanza pia aliipa kazi na kusababisha hasara kubwa.
Akitoa mwongozo, mwenyekiti wa kikao Mhe. Mussa Azzan Zungu ametupia lawama serikali kwa kutosikiliza malalamiko ya wananchi na kuwahamisha viongozi wabovu wanaotenda makosa toka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine.
Wakati huohu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid amewasilisha kauli ya serikali Bungeni kuhusu hali ya Dawa na matibabu ya saratani, ambapo amesema serikali imelipa shilingi bilioni 21 kwa Bohari kuu ya Dawa na sasa ina kamilisha uhakiki wa Deni la shilingi Bilioni 81 ili iweze kufanya malipo na kuagiza Bohari kuu ya Dawa kupeleka Dawa zenye thamani ya shilingi milioni 200 katika hospitali ya Muhimbili.
Katika hatua ngingine, Bunge limepitisha azimio la kuridhia itifaki ya kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki litakayosaidia nchi za Afrika kushirikiana katika kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali.