Jumanne , 24th Nov , 2020

Zaidi ya mwaka mmoja tangu mtoto Rehema Hussein, kutoweka nyumbani kwao mtaa wa Nyerere, Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, katika mazingira ya kutatanisha akiwa na miaka 4 na wazazi wake kumtafuta bila mafanikio,hatimaye amepatikana akiwa na miaka 5 huku afya yake ikionekana kudhoofu.

Mtoto Rehema Hussein, aliyekuwa amepotea.

Wakizungumza na EATV wazazi wa mtoto huyo Hussein Masoud na Masha Kabwali, wamesema kuwa taarifa za mtoto wao kupatikana awali walipewa na aliyekuwa jirani yao, kwamba amemuona mtoto wao mtaa wa Kaparangawe, ulioko mkoani Katavi ijapokuwa hakuwa na uhakika.

Wazazi wa mtoto huyo wameongeza kuwa mtu aliyekuwa na binti yao, hata baada ya wao kufika na vielelezo mbalimbali ikiwemo picha na kadi ya kliniki, aliendelea kumng’ang’ania mtoto huyo huku akidai kuwa ni mwanae mpaka jeshi la polisi lilipoingilia kati, na mara baada ya uchunguzi pia lilibaini kuwa mtoto huyo hakuwahi kufanyiwa ukatili wa aina yoyote

Aidha mwanaume huyo mara baada ya kufanyiwa mahojiano, alidai kuwa mtoto huyo alipelekewa na mke wake anayeishi mkoani Tabora, na jeshi la polisi linaendelea kumshikilia kwa uchunguzi zaidi.