Alhamisi , 13th Feb , 2025

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeitaka Serikali kukamilisha upelelezi kwa wakati, kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai pekee yake.

Boniface Jacob, mwenyekiti CHADEMA, kanda ya Pwani

Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter) katika Mahakama mahakama hiyo.

 

Kesi hiyo ilipangwa jana Jumatano Februari 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangaliwa iwapo upande wa mashtaka umekamilisha upelelezi au laa, lakini Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

 

Mbilingi baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi Peter Kibatala amedai ana mambo mawili ya kuzungumza, moja ni kwamba upande wa mashtaka hauko makini na suala ya upelele. Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, alielekeza upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo kwa haraka ili iweze kuendelea na hatua nyingine.

 

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

 

Katika shtaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).

 

Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake.

 

MWISHO.